VIONGOZI ambao wametawala siasa za Kenya kwa miongo kadhaa wanakabiliwa na swali gumu huku uchaguzi mkuu wa Agosti 2027 ukikaribia: Je, wako tayari kukabidhi hatamu kwa kizazi kipya au wataendelea kupigania nafasi zao katika uongozi?
Miongoni mwa wanasiasa wanaokabiliwa na mjadala huo ni Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya, Martha Karua, kiongozi wa ODM Oburu Oginga, Gavana wa Siaya James Orengo na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale.
Wachanganuzi wanasema ingawa viongozi hao bado wana mitandao mikubwa ya kisiasa, uzoefu na ushawishi katika maeneo yao, wanakabiliwa na shinikizo kutoka kwa vijana wanaotaka mabadiliko ya kizazi katika uongozi.“Mjadala si kwamba viongozi hawa wameishiwa na ushawishi wa kisiasa.
Wengi bado wana mitandao, uzoefu serikalini na uwezo wa kujadiliana kuhusu miungano.
Swali ni iwapo mifumo iliyowadumisha madarakani kwa miaka mingi inaweza kustahimili kiu ya mabadiliko ya kizazi,” anasema mchambuzi Geoffrey Mboya.
Mabadiliko hayo yanajitokeza wazi katika eneo la Magharibi mwa Kenya, ambako baadhi ya wanasiasa wakongwe wameunga mkono azma ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwania urais.
Waliokuwa mawaziri Musikari Kombo, Fred Gumo, Noah Wekesa na Philip Masinde, pamoja na wabunge wa zamani Joash Wamang’oli na Bifwoli Wakoli, wamejitokeza kuunga mkono Sifuna, wakisema eneo hilo linahitaji kuandaa kizazi kipya cha viongozi wa kitaifa.