MASHIRIKA ya kutetea haki za binadamu yamekosa ruhusa ya kukagua eneo la Ikulu ya Nairobi, kufuatia madai kuwa ujenzi wa kanisa lenye thamani ya Sh1.8 bilioni unakaribia kukamilika licha ya agizo la korti la kusimamisha mradi huo.
Jaji David Mburu alitupilia mbali ombi hilo, akisema mashirika hayo hayakuwasilisha ushahidi wowote wa kuhalalisha ukaguzi wa eneo hilo.
Alisema mahakama haiwezi kutumiwa kufanya uchunguzi kwa niaba ya walalamishi.
Mashirika hayo ni Transparency International Kenya, Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu, Inuka Kenya Ni Sisi na Taasisi ya Uwajibikaji wa Kijamii.
Mashirika hayo yaliiambia mahakama kuwa yalipokea taarifa za ndani kwamba ujenzi wa kanisa hilo ulikuwa karibu kukamilika, hatua ambayo huenda ilikiuka agizo la mahakama la Agosti 26, 2025.
Kesi hiyo iliwasilishwa Agosti 2025, mashirika hayo yakipinga mpango wa kujenga kanisa la kudumu katika Ikulu.
Yalisema mradi huo unakiuka Katiba kuhusu kutengwa kwa masuala ya dini na utawala, matumizi ya ardhi na rasilimali za umma, usawa, uhuru wa kuabudu na ushirikishaji wa wananchi.
Wakili wa walalamishi alisema duru za kuaminika ziliwaarifu kuwa kanisa hilo lilikuwa karibu kukamilika.
Aliomba mahakama iruhusu ukaguzi kubaini iwapo ujenzi ulikuwa umeendelea licha ya amri iliyopo.
Alisema walalamishi wangeondoa kesi hiyo iwapo kanisa lilikuwa limekamilika, lakini hawakuweza kupata ushahidi kwa kuwa Ikulu inalindwa na haifikiki kwa urahisi.