WANAWAKE ni wengi katika makanisa ya Kavonokya lakini hawana nafasi kubwa ya kutoa maoni yao.
Wanatakiwa kufunika vichwa kwa vitambaa vinavyoziba masikio na kuvaa magauni marefu yenye mikunjo.
Kujipodoa, kucha bandia na urembo wa kisasa haviruhusiwi. Hata wanapotaka kutoa maoni yao kanisani, wanawake wanapaswa kuyawasilisha kupitia waume zao.
“Mwanamke wa Kavonokya anayetaka kutoa hoja kanisani hawezi kufanya hivyo moja kwa moja. Anapaswa kuitoa kupitia mumewe,” anasema Mulyungi Ndithya, mhubiri katika kanisa la Kavonokya karibu na mji wa Mwingi, Kaunti ya Kitui.
Viongozi wa madhehebu hayo pia wanawataka wanaume kuwaoa wanawake wanaoshiriki imani hiyo ili kuilinda dhidi ya ushawishi wa dini zingine.
Hata hivyo, masharti kuhusu ndoa, matumizi ya dawa za hospitalini na kupiga kura yamewafanya baadhi ya vijana kujiondoa katika madhehebu hayo.
Kwa Vundi Masai, kifo cha mkewe Faith Kumbwa mnamo 2019 kilimfanya kuachana na Kavonokya baada ya miaka 34. Mkewe alipougua akiwa mjamzito, alianza kwa kutafuta maombi kutoka kwa wazee wa kanisa.
Hata hivyo, hali yake ilipozidi kuwa mbaya, alimpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Mwingi, ambako alifariki licha ya juhudi za madaktari kumwokoa.
“Kavonokya ilinikatisha tamaa nilipoihitaji zaidi,” akasema Bw Masai, ambaye sasa amejiunga na Kanisa la African Inland Church (AIC).
Rose Mutua pia alipinga mafundisho hayo baada ya kuolewa na Willy Kamuti mnamo 1994. Alimpa mumewe sharti la kuchagua kati ya ndoa na Kavonokya.