MAHAKAMA kuu imeratibisha kuwa dharura kesi ya kuzima tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kuipa kampuni ya Amerika –Smartmatics International Holdings B.V zabuni ya Sh17.6 bilioni kutengeneza vifaa vya kieletroniki vya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Kesi hii imewasilishwa kortini siku moja baada ya aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua kudai kandarasi ya ununuzi wa vifaa hivi vya kura almaarufu KIEMS kati ya IEBC na kampuni ya Amerika inatamatika Novemba 24, 2026 (Jumanne).
Jaji David Mburu alisema kesi hiyo iliyowasilishwa na Mabw Koome Kevin na Zedekiah Samson imezua masuala mazito ya kisheria na kwamba inapasa kuamuliwa pasi na kusita.
Jaji Mburu alimwagiza wakili Elly Okoth aliyewasilisha kesi chini ya sheria za dharura aikabidhi IEBC nakala za kesi hiyo mnamo Novemba 24, 2026 na kuiamuru tume iwasilishe ushahidi kujibu madai kwamba imeshikana na kampuni inayokabiliwa na madai ya ufisadi wa kimataifa.
Jaji huyo aliamuru kesi hiyo itajwe Novemba 30, 2026 kwa maagizo zaidi.
Akiwasilisha ushahidi, Bw Okoth alimweleza jaji huyo kwamba kampuni ya Smartmatics inakumbwa na kashfa za ufisadi hata imeshtakiwa katika nchi ya Ufilipino kwa ufisadi wa USD ($)1 milioni.
Inadaiwa kampuni hiyo ya Smartmatics ilimlisha mlungula aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wa Ufilipino kwa kuipa kandarasi ya vifaa vya kieletroniki vya kupiga kura.