WAKULIMA wanawake nchini wanazalisha mapato mengi kwa kila hekta kuliko wanaume, lakini wanashindwa kupata faida inayolingana kutokana na ukosefu wa mikopo nafuu na vifaa vya kisasa vya kilimo.
Tathmini ya miaka tisa iliyofanywa na Farm to Market Alliance (FtMA), imeonyesha kuwa wanawake hupata wastani wa Sh82,494 kwa hekta wakati wa msimu mkuu wa kilimo, ikilinganishwa na Sh69,833 wanazopata wanaume.
Hata hivyo, vituo vya huduma za wakulima vinavyoongozwa na wanawake hupata faida ya wastani wa Sh143,989 kwa mwaka, ikilinganishwa na Sh515,253 kwa vituo vinavyoongozwa na wanaume.
Ripoti hiyo inasema tofauti hiyo inachangiwa na changamoto za kupata fedha na vifaa vinavyohitajika kupanua biashara za kilimo.
Kwa wastani, vituo vinavyoongozwa na wanawake vina vifaa viwili pekee, ikilinganishwa na 3.2 katika vile vinavyoongozwa na wanaume.
Hali hii inapunguza uwezo wao wa kutoa huduma za mashine, kushughulikia mazao mengi na kuyahifadhi baada ya mavuno.
Mratibu wa FtMA nchini, George Njoroge, alisema matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanawake na vijana wanaweza kupata mapato zaidi wakipata mbegu bora, mafunzo na masoko ya uhakika.
Alisema ni muhimu kuondoa vikwazo vinavyozuia wakulima hao kupanua shughuli zao.
Ripoti hiyo pia ilibaini kuwa asilimia 70 ya vituo vya huduma za wakulima havina mikopo kutoka taasisi rasmi, licha ya asilimia 97 kuwa na akaunti za benki.
Masharti ya mikopo yanayohitaji wakopaji kutoa ardhi kama dhamana yanatajwa kuwa kikwazo kikuu, na kulazimisha baadhi ya…

