MVUTANO unaendelea kutokota ndani ya chama cha ODM kuhusu ushirikiano wake na chama tawala cha UDA, huku ushindani wa tiketi za uchaguzi na kuimarika kwa chama cha MDG vikiibua wasiwasi kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.
Hali hii inajiri huku kiongozi wa ODM Oburu Oginga akisisitiza kuwa chama hicho kitabaki imara na kuendeleza ushirikiano na Rais William Ruto, lakini baadhi ya viongozi wanataka hakikisho kuwa ODM haitapoteza uhuru wake wala maslahi ya kisiasa.
Katika mkutano wa Kamati Kuu ya ODM jana, chama hicho kiliweka Januari 31, 2027 kuwa tarehe ya mwisho ya kukamilisha mazungumzo na UDA kuhusu manifesto ya pamoja itakayoweka msingi wa muungano unaopendekezwa.
Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed alisema pande hizo mbili zinapaswa kukubaliana kuhusu sera na masuala yatakayowaunganisha kabla ya uchaguzi.
"Tunataka kupokea ripoti ifikapo Januari 31 kuhusu masuala na sera zitakazotuunganisha iwapo tutaunda muungano na UDA. Tutashirikiana kuendeleza ajenda ya Wakenya," alisema.
Oburu, ambaye alikuwa akimpokea aliyekuwa Mbunge wa Bureti Paul Sang aliyejiunga na ODM kutoka Kanu, alisisitiza kuwa chama hicho hakitaruhusu watu wa nje kukivuruga.
Alisema waliohama vyama vingine na kujiunga na ODM hawatapewa tiketi za moja kwa moja, bali watashindana na wanachama wengine katika kura za mchujo.
"Hakuna mtu aliye na upendeleo maalumu ndani ya ODM. Kila mtu atashindana na mwenzake.