Vyama 94 vya kisiasa nchini vimepewa hadi Desemba 7, 2026 kurekebisha kanuni zao za uteuzi wa wagombeaji, la sivyo vikose kushiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesema ni vyama 11 pekee vilivyotimiza masharti ya kisheria kuhusu kanuni za uteuzi, huku vingine 94 vikihitajika kufanya marekebisho.
Miongoni mwa vyama vikuu vilivyotakiwa kurekebisha kanuni hizo ni United Democratic Alliance (UDA) ya Rais William Ruto, Orange Democratic Movement (ODM), Democracy for the Citizens Party (DCP) ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Linda Mwananchi Movement, iliyokuwa ikijulikana kama The Equitable Party.
Hata hivyo, Wiper Patriotic Front ya Kalonzo Musyoka, Jubilee Party na The Mwananchi Party ya Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ni miongoni mwa vyama 11 vilivyotimiza masharti.
Vyama vingine vilivyofaulu ni Kenya Moja Movement, Safina, Liberal Democratic Party, Grand Dream Development, Democratic National Alliance, Chama ya Mapatano of Kenya, Vision for Development Alliance na Forward Kenya.
Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alisema tume ilikagua kanuni zilizowasilishwa na vyama ili kuhakikisha zinafuata Katiba, Sheria ya Uchaguzi na kanuni husika.
Alisema tathmini hiyo ilichunguza muundo na mamlaka ya kamati za uchaguzi za vyama, taratibu za kutambua na kuteua wagombeaji, masharti ya wanaotaka kuwania nafasi za uongozi na jinsi kura za mchujo zinavyopaswa kuendeshwa.