WAJIBU wa wazazi katika kuwalinda watoto ulikuwa kiini cha hukumu iliyotolewa Jumanne na Mahakama ya Watoto Mombasa dhidi ya mhubiri mtatanishi Paul Mackenzie na wafuasi wake kuhusu ukatili dhidi ya watoto katika msitu wa Shakahola kati ya 2020 na 2023.
Hakimu Mkuu Nelly Chepchirchir alisema ushawishi wa Mackenzie kwa wafuasi wake haukumfanya moja kwa moja kuwajibika kwa kila ukiukaji wa haki za watoto, akisisitiza kuwa kila mshtakiwa alipaswa kuhusishwa na kosa mahususi.
"Ushahidi dhidi ya kila mshtakiwa ulizingatiwa kivyake. Ukubwa wa matukio au umaarufu wake hauwezi kuchukua nafasi ya kuthibitisha hatia," alisema hakimu.
Mahakama ilisema wazazi waliowapeleka watoto wao msituni walikuwa na wajibu wa kuwalinda, huku upande wa mashtaka ukishindwa kuthibitisha kuwa Mackenzie alikuwa na wajibu wa moja kwa moja wa malezi ya watoto hao.
Hata hivyo, hakimu alikataa hoja za utetezi kwamba vitendo vilivyofanyika vilichochewa na imani za kidini au vilikuwa njia ya kuwaadhibu watoto.
Alisema uhuru wa kuabudu hauwezi kutumiwa kuhalalisha vitendo vinavyodhuru watoto.
Mackenzie alipatikana na hatia ya kushambulia kulikosababisha madhara ya mwili na makosa matano ya kuwafanyia watoto ukatili.
Washtakiwa wengine kadhaa walipatikana na hatia ya ukatili na kuwanyima watoto haki ya elimu.
Washitakiwa wengine 24 waliachiliwa huru baada ya mahakama kubaini kuwa mashtaka hayakuthibitisha wajibu wao binafsi.
Mackenzie na washitakiwa wenzake wanatarajiwa pia kusikiliza hukumu katika kesi ya itikadi kali katika Mahakama ya Shanzu Alhamisi…