BAADA ya takriban miaka tisa ya mazungumzo, maafisa wa utabibu hatimaye walipata makubaliano ya pamoja (CBA) kuhusu masuala waliyoibua, lakini sasa wanatishia kugoma wakidai serikali za kaunti hazijatekeleza makubaliano hayo.
Katibu Mkuu wa Muungano wa Maafisa wa Utabibu nchini (Kuco) George Gibore, amesema chama hicho kimetoa notisi ya siku saba kwa Baraza la Magavana, Wizara ya Utumishi wa Umma, serikali za kaunti na Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), wakitaka utekelezaji wa makubaliano hayo uanze mara moja.
Alisema kucheleweshwa zaidi kwa utekelezaji kutawalazimu wanachama kurejea kwenye mgomo.
Mazungumzo kuhusu CBA yalianza mwaka 2017 na makubaliano yalifikiwa mwaka jana. Kaunti zote zilialikwa kutia saini mkataba huo pamoja na makubaliano ya kurejea kazini baada ya mgomo.
Hata hivyo, baadhi hazikutia saini.
"Tumekuwa tukikabiliwa na uhasama katika kaunti nyingi," alisema Bw Gibore.
Maafisa hao waligoma Julai mwaka huu, na kaunti nyingi zikakubali kutia saini makubaliano hayo.
Hata hivyo, Nairobi, Vihiga, Kakamega, Turkana na Uasin Gishu bado hazijatia saini.
Kwa mujibu wa Bw Gibore, baadhi ya wanachama katika kaunti hizo wameendelea kugoma kwa zaidi ya siku 100.
Alilitaka Baraza la Magavana kuhakikisha kaunti zote zinatia saini mikataba hiyo na kuitekeleza.
Miongoni mwa masuala yaliyokubaliwa ni kuongezwa kwa marupurupu ya hatari kazini, kupitiwa upya kwa mishahara na kuboreshwa kwa mwongozo wa kupandishwa vyeo.