TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) itaanzisha mfumo wa kuwapa wanahabari taarifa zitakazowawezesha kuchunguza uadilifu na sifa za wanaotaka nyadhifa za uchaguzi na uteuzi kabla ya uchaguzi wa 2027.
Mwenyekiti wa EACC David Oginde alisema mpango huo utasaidia wanahabari kuchunguza historia, mwenendo na rekodi za wagombea badala ya kutegemea ahadi za kampeni na miungano ya kisiasa.
Akizungumza katika mkutano wa tisa wa wahariri nchini, uliofanyika Travelers Beach Hotel, Mombasa, Alhamisi, Dkt Oginde alitaja vyeti ghushi, hongo ya wapiga kura, matumizi mabaya ya rasilimali za umma na ghasia za kisiasa kuwa baadhi ya maovu yanayohitaji uchunguzi zaidi.
Alisema EACC itaimarisha ufuatiliaji na uchunguzi wa hongo ya wapiga kura, akiwataka wanahabari kuelimisha wananchi kuhusu madhara yake kwa demokrasia.
“Hongo ya wapiga kura inadhoofisha uhuru wa wananchi kuchagua viongozi wao. Inageuza uamuzi muhimu wa kidemokrasia kuwa biashara,” alisema.
Pia aliwaonya maafisa wa umma dhidi ya kutumia magari, fedha, wafanyakazi na shughuli za serikali kujinufaisha kisiasa, akisisitiza kuwa wanaotaka kugombea lazima wajiuzulu angalau miezi sita kabla ya uchaguzi.
Dkt Oginde alilaani matumizi ya vijana kuchochea ghasia na vitisho wakati wa kampeni, akisema wanaopanga na kufadhili vurugu lazima wawajibishwe.
Rais wa Kenya Editors Guild Zubeida Kananu aliwataka wanahabari kuchunguza jinsi wagombea walivyoishi, walivyohudumu na wanavyofadhili kampeni zao.