Aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado amehukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kwa mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno na mtoto wake ambaye hakuwa amezaliwa mwaka 2018.
Mahakama Kuu ya Milimani pia ilimhukumu aliyekuwa msaidizi wake wa kibinafsi Michael Juma Oyamo kifungo cha miaka 25, huku aliyekuwa mfanyakazi wa serikali ya kaunti ya Migori Caspal Ojwang Obiero akifungwa miaka 18.
Hukumu hizo zilitolewa na Jaji Cecilia Githua jana.
Sharon alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Rongo akisomea stashahada ya afya ya tiba. Alikuwa na ujauzito wa miezi saba alipopatikana ameuawa Septemba 2018. Pia alikuwa na watoto watatu kutokana na uhusiano wake wa awali.
Mamake Sharon, Melinda Auma Rangili, aliambia mahakama kuwa bintiye alikuwa amemweleza kuwa Obado ndiye aliyempa mimba. Uchunguzi wa DNA ulithibitisha kuwa Obado ndiye baba wa mtoto huyo, jambo ambalo alikubali mahakamani. Alisema alikuwa na uhusiano na Sharon na kwamba mtoto aliyekuwa amebeba tumboni alikuwa wake.
Katika uamuzi uliotolewa Julai 23, mahakama iliwapata wanaume hao watatu na hatia ya mauaji baada ya kusikiliza mashahidi 42 wa upande wa mashtaka na kupokea vielelezo 81.
Jaji Githua alikubaliana na ushahidi wa upande wa mashtaka kuwa Obado ndiye aliyekuwa na sababu ya kupanga mauaji hayo na kutoa fedha, Oyamo alisaidia kutekeleza mpango huo, huku Obiero akitoa msaada wa usafirishaji na kuficha uhalifu huo.