Je, haki imetendeka hatimaye katika mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno, au adhabu iliyotolewa ni hafifu ikilinganishwa na uzito wa kosa? Hili ndilo swali linaloibua mjadala baada ya aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado kuhukumiwa kifungo cha miaka 25 jela.
Baadhi ya Wakenya na mashirika ya kutetea haki za binadamu wamesema adhabu hiyo ni ndogo, wakiamini Obado na washirika wake walistahili vifungo vikali zaidi kutokana na mauaji ya Sharon aliyekuwa mjamzito.
Hata hivyo, familia ya Sharon imesema itakata rufaa ikitaka Obado aachiliwe huru. Wakili wake, Antony Opondo, alithibitisha hatua hiyo. Kikosi cha mawakili wake pia imesema itakata rufaa kupinga uamuzi huo.
Obado alihukumiwa Ijumaa kifungo cha miaka 25 kwa mauaji ya Sharon, aliyekuwa mpenzi wake. Aliyekuwa msaidizi wake wa kibinafsi, Michael Oyamo, naye alipata miaka 25, huku aliyekuwa karani wa Kaunti ya Migori, Caspal Obiero, akihukumiwa miaka 18.
Shirikisho la Wanasheria Wanawake nchini (FIDA-Kenya) lilipongeza uamuzi huo, likisema ni hatua muhimu katika kuwawajibisha wahusika na kuhakikisha waathiriwa wanapata haki.
Mwenyekiti wa FIDA Christine Kungu alisema hukumu hiyo imehitimisha hatua muhimu katika harakati za miaka karibu minane za familia ya Sharon kutafuta haki.
Alisema hakuna hukumu inayoweza kurejesha maisha ya Sharon na mtoto wake ambaye hajazaliwa, wala kuondoa maumivu ambayo familia imepitia.
Gavana wa sasa wa Migori Ochilo Ayacko alisema amefuatilia kwa wasiwasi hukumu dhidi ya mtangulizi wake na…