Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru amejitosa rasmi katika kinyang’anyiro cha kuwania wadhifa wa Naibu Rais unaoshikiliwa kwa sasa na Kithure Kindiki katika uchaguzi mkuu wa 2027, akisema yuko tayari kuwa mgombeaji mwenza wa Rais William Ruto.
Waiguru alisema huu ni mwaka wa tatu akijaribu kuwania nafasi hiyo, baada ya juhudi zake mbili za awali kutofanikiwa. Sasa amewataka washirika wake kuanza kampeni za kumshawishi Rais amchague kuwa naibu wake.
Alisema jamii ya Mlima Kenya inastahili uwakilishi wa kutosha katika uongozi wa kitaifa na kwamba usawa wa kijinsia unapaswa kuzingatiwa katika nafasi za juu serikalini.
“Hii ni mara yangu ya tatu na ninaamini nitafanikiwa. Namuomba Dkt Ruto anizingatie kuwa mgombeaji mwenza wake katika uchaguzi mkuu,” alisema.
Akizungumza na viongozi wa mashinani kutoka eneobunge la Ndia katika eneo la Gacharu Ijumaa jioni, Waiguru alisema ana uzoefu unaomfanya astahili nafasi hiyo.
Alitaja kuhudumu kwake kwa mihula miwili kama gavana na kuwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) kama baadhi ya sifa zake, akisema rekodi yake ya maendeleo inajieleza.
“Nimejaribiwa na kuthibitishwa. Nimekuwa gavana kwa mihula miwili na mwenyekiti wa Baraza la Magavana. Ninafaa kuwa Naibu Rais, na watu wangu wanapaswa kuwa na ujasiri wa kumwambia Rais hilo atakapozuru eneo hili,” alisema.
Waiguru pia aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kutounga mkono upinzani katika uchaguzi wa 2027 kwa sababu ya mzozo kati ya Rais Ruto na…